Sura Ya Kwanza

29 0 0
                                    

Mzee Moja ni pandikizi la mwanaume.

Huvalia kaptura na kabuti ndefu zinazomfika magotini.

Malaika zimemsimama miguuni pengine kumkingia kijibaridi cha jioni.

Miguuni amavaa viatu wazi vilivyotengenezwa kutokana na magurudumu makuukuu,kwa umaarufu 'Akara'.

Mkononi hupenda kubeba mkongojo maalumu wenye kidude cha kuchomoa kisu chenye ncha kali,patukiapo haja.

Fununu husema pia ni mumiliki wa bastola iliyoidhinishwa na vyombo vya usalama.

Sijui bastola ni ya kulindia maisha yake au kulindia mali yake!

Ni mcheshi ila meno yake yameharibika kwa kuvuta sigara.

Anapocheka kwa kwekwe zake ,meno huyasukuma madevu yaliyomkaba usoni na kuonekana.

Daima yuwapapasapapasa madevu haya,hasa wakati anapozungumza au kutafakari.

Kwa umbali uonekana kama mbweha aliyemuuma kifaranga mweupe kinywani kwa weupe wa ndevu hizi.

Weupe huu ni ishara tosha kuwa amebugia chumvi kiasi cha haja.

Kichwani amekuza nywele za kirasta.

Ni mufuasi wa Kirastafariani.

Kinyume cha ndevu,nywele zake ni nyepesi na nyeusi tititi!

Nyepesi na ndefu hivi kwamba zinaweza kutumika kama kamba kufungia kuku miguuni.

Anapotembea huchechemea kutokana na jeraha alilopata, wakati mmoja kwa kuanguaka kutoka kwa mti wa muembe.

Ujana una kishindo eti!

Mzee Moja alipenda sana kufuga tangu jadi za ubarobaro wake.

Kwa sasa ni mfugaji wa wanyama tofauti.

Usiseme ndege,ng'ombe,mbuzi,kondoo na punda.

Ana njiwa aliowafuga na hupendelea sana kuwapatia mtama nyakati za asubuhi kabla ya kuelekea ofisini,ama ukipenda hotelini mwake.

Wengine huruka na kumtua mabegani na kudona kutoka kwa viganja vyake.

Bila shaka hustarehe na kumwachia kinyesi rojorojo kikimtiririka mgongoni.

Huepuka kadhia hio kwa kuvalia gwanda maalum kumkingia nguo zisichafuliwe.

Mbona Mzee Moja kuchechemea?

Alikuwa ameukwea mwembe kuwachukua kinda wa njiwa ili kuwafuga kwake.

Kwa bahati mbaya tawi lililokumbatia kiota walimojisitiri kinda hao,lilikataa kuhimili uzito wa mwili wake na kumlaza ardhini kichwa ngoma.

Nusura kupasuka kichwa kwa kisiki kilichomkondolea macho chini ya mwembe.

Alikiepuka kwa bahati tu!

Alilazwa hospitalini kwa muda wa mwezi mzima.

Hivyo ndivyo alivyoanza kutembea akidensi,kama anavyopenda kujitania.

Lakini si kuchechemea kwa kisawe kingine chochote bado ni kuchechemea tu?

Ni mzee mwenye utajiri mkubwa.

Utajiri wa mali wala si wa hali.

Kinyume na matarajio ya jamii,mzee huyu huishi maisha ya kawaida yasiyo madoido yoyote.

Hamnazo kawaachia kina Majivuno na Kivuto wanaopenda kuendesha magari aina ya Rangerover na kutembea kwa madaha,simu mbili mbili mikononi.

Mikufu na saa za dhahabu ama ukipenda bling bling,ndio zao

HIMAYA YA MZEE MOJAWhere stories live. Discover now